4 Mei 2023 - 11:56
Jaribio la Ukraine la kumuua Rais Putin wa Russia ndani ya Kremlin limefeli

Russia imeituhumu Ukraine kwa kujaribu kufanya jaribio la kumuua Rais Vladimir Putin katika shambulizi la Jumanne usiku dhidi ya Ikulu ya Kremlin kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Taarifa za jariibio hilo la kumuua Putin limetangazwa Jumatano na serikali ya Russia na kuripotiwa na mashirika kadhaa ya habari ya serikali.

Maafisa wa Russia wanasema Putin hakujeruhiwa na hakukuwa na uharibifu ndani ya Kremlin kufuatia hujuma hiyo.

Kremlin ilionya kwamba Russia ina haki ya kulipiza kisasi na kwamba inalitazama shambulio hilo kama shambulio la "kigaidi".

Shirika la Habari la kiserikali la RIA Novosti limeripoti kwamba, "Kremlin imetathmini vitendo hivi kama kitendo cha kigaidi kilichopangwa cha kujaribu kumuua Rais Putin wakati wa kukaribua Gwaride la Siku ya Ushindi Mei 9." Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa Rais Putin hajabadilisha ratiba yake na alikuwa akifanya kazi kama kawaida.

Aida imedokezwa kuwa Rais Putin hakuwa katika Ikulu ya Kremlin wakati wa hujuma hiyo na kwamba siku ya Jumatano alikuwa akifanya kazi katika makazi yake ya Novo Ogaryovo nje ya Moscow.

Video ambayo haijathibitishwa inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ya Russia, ikiwa ni pamoja na kanali ya Telegram ya chombo cha habari cha kijeshi Zvezda, ilionyesha moshi mweupe ukipanda nyuma ya jumba kuu la Kremlin baada ya tukio hilo.

Video hiyo ilitumwa mapema Jumatano kwenye kikundi cha wakaazi wa kitongoji kilicho mkabala wa Kremlin katika Mto Moskva na kusambazwa na vyombo vya habari vya Russia.

Wakati huo huo siku ya Jumatano, meya wa Moscow Sergei Sobyanin alitangaza kupiga marufuku safari za ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Russia.

Sobyanin amesema hatua hiyo itazuia "matumizi haramu ya ndege zisizo na rubani ambazo zinaweza kuzuia kazi ya utekelezaji wa sheria".

Mbunge anayewakilisha Crimea huko Moscow, Mikhail Sheremet, aliambia vyombo vya habari vya serikali ya Russia kwamba Kremlin inapaswa kuamuru shambulio la kombora kwenye makazi ya Rais wa Ukraine Zelenskyy huko Kyiv kulipiza kisasi jaribio hilo la kumuua Rais Putin.

342/